RISARA
YA MGENI RASMI MBUNGE WA VITIMAALUMU ROSE TWEVE SIKU YA WANAWAKE 08/03/2015
KIJIJI CHA IGOWOLE WILAYA YA MUFINDI
Ndugu
Viongozi mbalimbali wa Vyama vya Siasa, Watendaji
wa Serikali na Asasi za Kiraia, Viongozi
wa Jumuiya za Dini, Waandishi
wa Habari, Wakina
Mama wote, Wageni waalikwa, Mabibi
na Mabwana.
Ndugu viongozi na wananchi wote mliohudhuria.Napenda
kuchukua fursa hii kuushukuru uongozi wa Wilaya ya Mufindi pamoja na Viongozi wote wa Serikali kwa ujumla
kwa maandalizi mazuri kufanikisha shughuli hii ya Maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani mwaka huu 2016 inayofanyika kiwilaya hapa Igowole.
Niwashukuru kwa dhati wananchi wote wa wilaya
hii, kwa namna mlivyojipanga kwa kushirikisha akina mama, vikundi mbalimbali
vya sanaa na burudani kufanikisha Maadhimisho haya.
Aidha, nachukua nafasi hii kutoa
shukrani kwa Mashirika, Taasisi za Serikali na Mashirika yasiyo ya Kiserikali
ambao wametoa michango yao ya hali na mali katika kufanikisha maadhimisho haya.
Ndugu
wananchi Napenda nitoe shukrani za dhati
kwa kunipa heshima hii kubwa ya kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho
haya ya Siku ya Wanawake Duniani Kiwilaya ambayo leo tarehe 08/03/2016 yanafikia kilele chake.
Naomba nikiri, kwa vigezo mbalimbali
nilivyoona hapa, nalazimika kusema Maadhimisho haya kwa wilaya yamefana sana.
Hongereni sana.
Naamini ushirikiano wenu na wadau
mbalimbali umewawezesha kufanikisha maadhimisho haya. Kama nilivyosema awali,
napenda kurudia tena kuvishukuru vikundi vya burudani, 2 vikundi vya kijamii na
Asasi mbalimbali kwa kujitokeza kwa wingi kuungana na wanawake katika
maadhimisho haya muhimu kwa Wanawake duniani.
Ndugu Viongozi na Wananchi Chimbuko la
Siku ya wanawake Duniani lilianza miaka mingi na mtakumbuka mwaka 1911 Wanawake
kule Nchini Marekani waliandamana kudai haki zao ambazo walikuwa wakizikosa:
kama vile kulipwa ujira mdogo, kufanyishwa kazi ngumu na kwa masaa mengi,
kukosekana kwa huduma za jamii na ubaguzi wa kijinsia.
Mara baada ya Umoja wa Mataifa
kuanzishwa mwaka 1945, lilipitishwa azimio kwamba tarehe 08 Machi ya kila mwaka
iwe ni Siku ya Maadhimisho ya Wanawake Duniani.
Kwa hiyo, tunapokutana hapa leo lengo
kubwa ni kukumbushana na kuweka mikakati zaidi ya kukabiliana na changamoto
mbalimbali zinazowahusu Wanawake. Miongoni mwa changamoto hizo ni unyanyasaji
wa kijinsia na athari za kiafya, wanawake kutopewa haki sawa katika maamuzi na
kutoshirikishwa. Wanawake katika jamii hutoa mchango mkubwa katika kutunza
familia, lakini bado wanaathirika zaidi na maradhi kama vile UKIMWI, vifo
vinayotokana na uzazi, kupigwa, kutukanwa, kutelekezwa, kubakwa, ukeketaji, mimba
za utotoni, kunyimwa haki ya kumiliki mali, n.k .
Hivyo, kukutana kwetu si kwa ajili ya
kufanya sherehe tu, pia ni kufanya tathimini kwa pamoja kutafakari namna gani
tumepiga hatua katika kukabiliana na changamoto za Wanawake au bado tuko
palepale.
Ndugu Viongozi na Wananchi, Serikali
yetu imejitahidi kuweka mikakati ya kutatua changamoto mbalimbali ili kuleta
usawa wa maendeleo na amani. Wananchi wamehamasishwa kupitia nyanja mbalimbali
kuhusu haki za Mwanamke na Mwanaume, kumiliki Ardhi, kuwaongezea wanawake uwezo
wa kiuchumi, kuwashirikisha wanawake kuhifadhi mazingira na kuwapa wanawake
nafasi za uongozi. Kama wengi wetu tunavyo fahamu nchi yetu sasa imepiga hatua
ya kuwa na kiongozi mwanamke katika ngazi za juu ambaye ni makamu wa Rais wa Jamuhuri wa Tanzania Samia Suluhu Hasani
hii yote ni kuonesha kuwa wanawake tunaweza na haki sasa inapatikana,Wanawake
pia wamehamasishwa kuhusu umuhimu wa kujiendeleza kielimu, kiuchumi kiafya kwa
kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo maambukizi ya VVU na UKIMWI, Saratani
ya Matiti na Shingo ya uzazi n.k.
Ndugu Viongozi na Wananchi, Leo hii
Duniani kote yanafanyika maadhimisho kama haya na Tanzania ni miongoni mwa
Mataifa ambayo yamekuwa mstari wa mbele kutambua mchango wa mwanamke, kuthamini
jitihada zake katika kuleta mafanikio na kuhamasisha mabadiliko ya jamii nzima.
Nchi yetu pia inatambua, umuhimu wa
mchango wa mwanamke katika shughuli za kisiasa, kijamii na kiuchumi. Hivyo,
mwaka huu wilaya ya Mufindi inaungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha Siku
ya Wanawake Duniani. Kauli mbiu ya mwaka huu“Pigania Haki na Usawa wa
Kijinsia”. Ujumbe huu unaelimisha na kuikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa
kubadili mtizamo uliopo na kuleta usawa kati ya jinsia zote kwa kuondoa dhuluma
mbalimbali za jinsia moja dhidi ya nyingine.
Pamoja nakuwepo mafanikio katika kuleta usawa
wa kijinsia hapa nchini na duniani kote, bado usawa kamili wa kijinsia
haujafikiwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile; mfumo dume wa maisha
uliopo katika baadhi ya maeneo, mila potofu miongoni mwa jamii na mtizamo hasi
kwa nafasi ya mwanamke 3 katika masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na
kiuchumi ambapo wanaume wamepewa nafasi kubwa na madaraka zaidi.
Athari za vitendo hivyo ni kuongezeka
kwa kasi ya UKIMWI, Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, ombaomba,
elimu duni, wakimbizi, ukosefu wa huduma hususan kwa Watoto.
Kijamii Wanawake huwa dhaifu na pengine
kuleta tamaa ya maisha na kuamua kujiingiza katika vitendo visivyofaa ikiwemo
ukahaba na hatimaye wengine kupata UKIMWI.
Hata hivyo, Serikali inaendelea kuchukua
juhudi za makusudi kuwawezesha wanawake kushiriki katika shughuli za kijamii
kielimu, kiafya na kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujasiriamali, uzalishaji na
usindikaji wa mazao.
Hivyo ni jukumu letu sote kutambua na
kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wanazidi kushikamana na kudumisha usawa
ndani ya familia ambako ndiko chimbuko la mambo yote ya mabadiliko na usawa wa
kijinsia.
Nina hakika mambo haya yakianzia katika
ngazi ya familia matokeo yake ni makubwa kwani hatimae jamii nzima itakuwa na
mtizamo wa pamoja na kutambua nafasi ya mwanamke kuwa sawa na mwanaume katika
nyanja mbalimbali.
Ndugu Viongozi na Wananchi, Napenda kusisitiza
Wanawake na Wanaume na jamii yote kwa ujumla tushirikiane kuchukua hatua zaidi
kuchochea mabadiliko miongoni mwetu ili kuhakikisha usawa wa kijinsia
unapatikana katika nyanja zote za Elimu, Afya Uchumi, Siasa, Ajira Utamaduni na
hata katika shughuli za biashara kwa ajili ya ustawi wa Wilaya,Mkoa na taifa
letu kwa ujumla. Mafanikio ya Mabadiliko haya yatapatikana iwapo jamii yote
wakiwemo wanaume kushiriki katika kupinga vitendo vinavyobagua jinsia nyingine.
Ndugu Viongozi na Wananchi Baada ya
kusema hayo, narudia kuwapongezeni sana, ninawatakieni kheri katika kuhitimisha
kilele cha Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Ki-Mkoa na Mwenyezi Mungu awabariki
sana.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni